Msajili wa Hazina atoa ufafanuzi

Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru ametoa ufafanuzi wa taarifa iliyosambaa  kuhusu msimamo  wa serikali kwa Benki ya Twiga Bancorp. Akizungumza jana, Dar es Salaam, Mafuru alisema benk hiyo ina changamoto za kimtaji haina maana  kwamba ipo kwenye hali mbaya kushindwa kujiendesha bali inahitaji nyongeza ya mtaji kwa ajili  ya kutekeleza matakwa ya kisheria katika usambazaji huduma nchini.

Alisema hatua hizo zinatokana na agizo la Rais Dk. John Magufuli kwa Katibu Mkuu  wa Wizara ya Fedha  na Mipango  la kutaka  kufuatilia  utendaji wa Benki ya Twiga Bancorp na kuhakikisha kasoro zilizopo zinatatuliwa.

“Kuna njia mbalimbali za kuiwezesha benki kupata mtaji  ikiwemo nje ya utaratibu  wa serikali, ndiyo maana Wizara ya Ofisi ya Msajili wa Hazina  ikishirikiana na manejimenti ya Twiga Bancorp  zinaandaa mapendekezo  yatakayoiwezesha benki hii kupata mtaji ili kuiwezesha kutimiza malengo yake,” alisema.

Mafuru alisema hatua mbalimbali  zilianza kuchukuliwa na Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Msajili wa Hazina  kwa ajili ya kuboresha  utendaji wa benki ya Twiga Bancorp ikiwemo kubadilishwa kwa muundo wake ambao pamoja na mambo mengine ulifanikisha kuteuliwa kwa menejimenti mpya.

Msajili huyo alisema kupitia menejimenti hiyo ulitengenezwa mpango mkakati wa miaka mitano ambo umeanza kutumika Januari mwaka huu. Mbali na hilo alisema serikali iliteua bodi mpya ya wakurugenzi.

Alisema kwa ujumla kuna mabadiliko makubwa ya kiutendaji baada ya hatua hizo kuchukuliwa.

“Hizi taarifa zinazosambaa kuwa benk inafungwa sio za kweli, kwenye benki kuna pesa za wananchi, kuna mkopo iliyotolewa kwa watu mbalimbali, kuna rasilimali za benki ikiwemo rasilimali watu.”

“Yote hayo yana utaratibu wake wa kuyasimamia hata ukisikiliza hotuba ya Rais hakusema funga Benki ya Twiga Bancorp aliagiza hatua zichukuliwe na kwamba Katibu Mkuu asimamie,” alisema.

 

Name of News Paper: Uhuru

Author: Anonymous        

Date:   Julai 19,2016