Benki ya Twiga Kutofungwa

Serikali  imetolea ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari kuhusu kufungwa kwa Benki ya Twiga  na kubainisha  kwamba benki hiyo  haitafungwa  na taarifa hizo zilieleweka vibaya. Akizungumza katika makao makuu ya benki hiyo Dar es Salaam jana, Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru alisema serikali inasubiri mapendekezo ya kitaalamu yatakayowezesha kutatua changamoto za kimtaji za Benki ya Twiga za Benki ya Twiga.

Mafuru alisema, anaposema changamoto za kimtaji hamaanishi kwamba  benki hiyo ipo kwenye hali mbaya  ya kushindwa  kujiendesha, ila inahitaji nyongeza ya mtaji  kwa ajili  ya kutekeleza matakwa ya kisheria na vile vile kuimarisha  na kusambaza  huduma katika maeneo mbalimbali ya nchi.

“Hatua hizi zinafuatia agizo alilolitoa Rais John Magufuli kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango kufuatilia utendaji wa Benki ya Twiga na kuhakikisha kasoro zilizopo zinatatuliwa,” alisema Mafuru.

Mafuru alisema kuna njia mbalimbali zinazochukuliwa za kuiwezesha  benki hiyo  kupata  mtaji, ikiwemo nje ya utaratibu wa serikali na wizara pamoja na Ofisi ya Msajili wa Hazina ikishirikiana na Menejimenti ya Twiga zinaandaa mapendekezo yatakayoiwezesha kupata mtaji wa kutimiza malengo ya kujiendesha kifaida.

Msajili  wa Hazina aliwakikishia wananchi kuwa fedha  zao zilizopo katika Benki ya Twiga  zipo salama na kwamba  uongozi uliopo unaendelea  kushughulikia  changamoto za kiutendaji zilizokuwepo kama alivyoagiza rais. 

 

Name of News Paper: Habari Leo

Author: Dennis Fussi       

Date:   Julai 19, 2016