Msimamo wa serikali juu ya Twiga Bancorp huu hapa.

Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, ametolea ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu msimamo wa serikali juu ya mwenendo mzima wa uendeshaji wa Benki ya Twiga Bancorp. Hatua hizo zinafutia agizo la Rais kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, kutaka uwepo  ufuatiliaji wa kuitendaji wa Benki hiyo  na kuhakikisha  kasoro zilizopo zinatatuliwa mara moja.

“Taarifa hiyo ilieleweka vibaya kuhusu msimamo wa Serikali kwa benki hii ya Twiga Bancorp. Naomba nieleze kwamba kwa hivi sasa serikali inasubiri  mapendekezo  ya kitaalamu yatakayowezesha kutatua  changamoto  za kimtaji  za Twiga Bancorp.

“Ninaposema  changamoto za kimtaji, sijasema kwamba benki hiyo ipo kwenye hali mbaya ya kushindwa kujiendesha yenyewe, ila inahitaji nyongeza ya mtaji kwa ajili ya kutekeleza matakwa  ya kisheria na vilevile kuimarisha  na kusambaza huduma mbalimbali katika maeneo  mengine ya nchi”, alisema  Mafuru.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, jana, Mafuru aliwaondoa wasiwasi watanzania akifafanua kuwa kuna aina mbalimbali za kuiwezesha benki kupata mtaji, tofauti  na baadhi ya watu wanavyofikiria.

“Kuna njia mbalimbali za kuiwezesha benki kupata mtaji ikiwamo nje ya utaratibu wa serikali. Ndiyo maana Wizara ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ikishirikiana na Manejimenti ya Twiga Bancorp zinaandaa mapendekezo  yatakayoiwezesha Benki hiyo kupata mtaji ili kuiwezesha kutimiza malengo  yake ya kiukuaji na kujiendeleza kwa faida.

Alisema, hatua mbalimbali zilianza  kuchukuliwa na Wizara ya Fedha  na Mipango  na Ofisi ya Msajili  wa Hazina kwa ajili ya kuboresha  utendaji wa Benki ya Twiga Bancorp.

“Kwa mfano, mnamo mwaka 2015, Muundo wa Shirika ulibadilishwa ambao pamoja na mambo mengine ulipelekea kuteuliwa kwa Manejimenti mpya.

Kwa kupitia Menejimenti hiyo mpya umetengenezwa Mpango Mkakati wa miaka mitano ambao umeanza kutumika tangu Januari mwaka huu kwa ajili ya kuleta ufanisi. Lakini pia, serikali ilifanya mabadiliko katika Bodi ya Wakurugenzi  na kuteua Bodi mpya ambayo itafanya kazi sambamba na mabadiliko mengine.

Kwa mujibu  wa Mafuru, hatua hiyo imeleta mabadiliko  makubwa   katika mchakato mzima wa kiutendaji wa benki hiyo,ikiwa ni pamoja na kuboresha zaidi huduma kwa wateja wake.

“Kwa ujumla kuna mabadiliko makubwa ya kiutendaji baada ya hatua hizo kuchukuliwa.Kwa mfano benki hiyo, imeweza kupata Hati Safi ya Mahesabu kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mara ya kwanza kwenye hesabu zake za mwaka 2015.Hili ni jambo ambalo halikuwezekana tangu Mwaka 2011.

“Hizi taarifa zinazosambaa kuwa benki inafungwa sio za kweli na ningependa kuwahimiza watanzania kuachana na taarifa hizo. Kwenye benki kuna pesa za wananchi, kuna mikopo iliyotolewa kwa watu mbalimbali, kuna rasilimali za benki ikiwemo rasilimali watu.

“Yote hayo yana utaratibu wake wa kuyasimamia. Hata ukisikiliza hotuba ya Rais, hakusema funga benki ya Twiga Bancorp aliagiza hatua zichukuliwe na kwamba Katibu Mkuu asimamie.

“ Kwa maelezo hayo, tunawahakikishia kuwa fedha za wananchi  zilizo  katika benk ya Twiga  Bancorp zipo salama na kwamba  uongozi  uliopo hivi sasa unaendelea kushughulikia changamoto za kiutendaji  zilizokuwapo  na kama yalivyokuwa maagizo ya Rais hatua mbalimbali  zimeanza kuchukuliwa  kwa ajili ya kuhakikisha mambo yote yanakuwa sawa.

Pia benki hii inaendelea kutoa huduma zake kwa wateja kama kawaida.” Alifafanua Mafuru.

Aidha  aliongezea kuwa, serikali itaendelea kutoa msukumo kwa benki hiyo  ili kuhakikisha tatizo lililopo sasa la mtaji linatatuliwa na kuhakikisha inajiendesha kwa faida na kuwanufaisha wateja wake.  

 

Name of News Paper: Raia Tanzania

Author: Anonymous

Date:  Julai 19, 2016